Makamu wa Rais wa Iran: Vituko vya Trump vimefika ukingoni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema zama za Rais Donald Trump wa Marekani na vituko vyake pamoja na timu yake inayopenda vita zimefika ukingoni.
Katika ujumbe kupitia Twitter, Eshaq Jahangiri, amesema taifa la Iran limesimama kidete mbele ya sera za Trump za mashinikizo ya hali ya juu kabisa. Amesema Trump amekuwa akiukiuka mikataba ya kimataifa ikiwemo ya mazingira na kiuchumi huku akiwawekea wananachi wa Iran vikwazo vilivyo dhidi ya ubinadamu sambamba na kuunga mkono ugaidi na ubaguzi wa rangi.
Jahangiri amesema wananchi wa Iran ambao wamesimama kidete mbele ya sera za Trump za mashinikizo ya juu kabisa katu hawatasahau masaibu yaliyosababishwa na sera hizo ambazo zimevuruga maisha ya kawaida, kupelekea watu wenye magonjwa sugu kukosa dawa na kuuawa kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran ameelezea matumaini yake kuwa sera haribifu za Marekani zitabadilika na nchi hiyo kuanza tena kuheshimu mataifa mengine na mikataba ya kimataifa.
Jana, vyombo kadhaa vya habari nchini Marekani viliripoti kwamba mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha Democratic nchini Marekani Joe Biden amechaguliwa kuwa rais wa 46 wa Marekani. Hata hivyo Trump amepinga matokeo hayo na kusisitiza kuwa kumekuwepo na wizi mkubwa wa kura.