Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran, muendelezo wa njama za aliyeshindwa
Baada ya Donald Trump kuitoa Marekani katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia yajulikanayo kwa jina la JCPOA hapo mwezi Mei 2018, Washington iliiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu na hadi leo hii, kila siku inaweka vikwazo vipya.
Jumanne usiku, tarehe 10 Novemba 2020, Trump alitangaza vikwazo vipya dhidi ya watu na taasisi zenye mfungamano na Iran. Wizara ya Hazina ya Marekani ilidai katika taarifa yake kwamba, imeiwekea vikwazo vipya kanali moja ya manunuzi yenye uhusiano na shirika la kijeshi la Iran. Taarifa ya wizara hiyo ilisema kuwa, leo ofisi ya kudhibiti mali za nje ya Wizara ya Hazina ya Marekani imeiwekea vikwazo kanali inayoundwa na mashirika 6 pamoja na watu wanne wanaohusika na manunuzi ya bidhaa muhimu na nyeti kwa ajili ya shirika la mawasiliano la Iran. Watu waliowekewa vikwazo hivyo vipya ni raia wa Iran na Taiwan.
Cha kusema hapa ni kwamba, hakuna kitu chochote cha maana kilichofanywa na serikali ya Trump hivi sasa kwani kwa muda mrefu nyuma, Marekani imekuwa ikiyawekea mashinikizo na vikwazo vya kila namna mashirika yenye mfungamano na Wizara ya Ulinzi na Sekta ya Ulinzi ya Iran. Hivyo ilichofanya sasa hivi Marekani ni kushadidisha tu vikwazo ilivyokuwa imeviweka tangu zamani. Vile vile vikwazo vya mara hii vinahusiana na watu ambao Washington inadai wanashirikiana na sekta ya mawasiliano ya Iran ambayo inadai ina mfungamano na Wizara ya Ulinzi ya Iran.
Inaonekana wazi kwamba hatua ya Trump ya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran ni ya kipropaganda tu na ni kuendeleza ukaidi wa kutokubali kushindwa kama ilivyo dhati yake Donald Trump. Kwa kuzingatia kuwa Trump amebwagwa katika uchaguzi wa rais wa Marekani uliofanyika tarehe 3 Novemba 2020, sasa hivi serikali yake imebakiwa na takriban miezi mwili tu hadi ianguke. Kwa mujibu wa viongozi wa ngazi za juu wa Marekani, Trump amekusudia kutumia muda huo uliobakia kuiwekea Iran vikwazo vya mfululizo, kiasi kwamba hata imedaiwa kuwa atakuwa anaweka vikwazo vipya kila wiki. Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, lengo kuu la serikali ya Donald Trump lilikuwa ni kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ili baada ya hapo irejeshe vikwazo vyote vya kimataifa vilivyoondolewa baada ya kufanikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Hata hivyo Marekani imefeli vibaya sana katika njama zake zote hizo mbili. Pamoja na hayo lakini, serikali ya Marekani inajifanya haikuathiriwa na fedheha iliyopata ya kususiwa na dunia nzima katika kampeni yake ya kutaka kurefusha vikwazo vya silaha na kurejesha vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran. Hivyo sasa hivi inatangaza vikwazo vipya ambavyo wachambuzi wa mambo wanasema, ni vya kipropaganda zaidi kuliko kuwa na chochote kipya ndani yake.
Mtandao wa habari wa Axios Jumapili usiku uliripoti kwamba serikali ya Trump itatumia muda mchache uliobakia wa serikali yake, kumimina vikwazo vya kila namna dhidi ya Iran ili kuizuia serikali ijayo ya Marekani isiweze kurejea katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA. Pamoja na njama zote hizo, lakini hivi sasa Marekani imetengwa zaidi kimataifa kuliko wakati mwingine wowote. Hii ni katika hali ambayo kwa upande wake, Iran imepata mafanikio ya kukabiliana vilivyo na vikwazo hivyo na kuvifelisha kupitia siasa zake za muqawama wa kiwango cha juu. Haydar bin Ali al Lawani, mhadhiri wa chuo kikuu na mchambuzi wa kisiasa raia wa Oman anasema: Marekani imedhoofika mno hivi sasa, huku Iran ikiimarika na kuwa dola kubwa lenye ushawishi wa kupigiwa mfano katika eneo hili.
Katika kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita, serikali ya Trump imechukua hatua zote mbaya na kali kadiri ilivyoweza dhidi ya Iran na sasa hivi wenyewe viongozi wa serikali ya Donald Trump wanakiri kwamba hakuna tena vikwazo vya kuweza kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Trump alikuwa ameahidi kwamba baada ya kujitoa katika mapatano ya JCPOA na kuiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu mno, angeliilazimisha Tehran ikubali kuburuzwa kwenye meza ya mazungumzo bila kutaka na itie saini makubaliano yoyote yanayotakiwa na Marekani. Hata hivyo amefeli vibaya katika njama zake hizo na ndio maana analaumiwa vikali ndani ya Marekani. Wanaomlaumu Trump wanasema kuwa, rais huyo mwanagenzi wa Marekani amefanya uanagenzi wa kuvamia mambo bila ya kuwa na stratijia maalumu na matokeo yake ameongeza tu wasiwasi baina ya Marekani na Iran, ameitoa Marekani katika njia yake na ameipotezea marafiki zake hata wa jadi. Hasa rais mteule wa Marekani, Joe Biden anamlaumu vikali Trump kwa kujitoa katika mapatano ya JCPOA, kwa kuikabili Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ya kuwa na mkakati wa maana na kuipotezea Marekani heshima na itibari yake kwa siasa zake mbovu zilizozitenga na Washington hata nchi za Ulaya ambazo ni waitifaki wa jadi wa Marekani.