Kiongozi Muadhamu atuma salamu za rambirambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Muhammad Yazdi
(last modified Thu, 10 Dec 2020 07:56:00 GMT )
Dec 10, 2020 07:56 UTC
  • Kiongozi Muadhamu atuma salamu za rambirambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Muhammad Yazdi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Muhammad Yazdi ambaye alikuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasomi na Wahadhiri wa Chuo cha Kidini cha Qum

Mwanazuoni maarufu wa Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Muhammad Yazdi, aliaga dunia jana na kurejea kwa Mola wake akiwa na umri wa miaka 89. Alitumua umri wake katika jihadi kwa ajili ya Uislamu na Mwenyezi Mungu.

Katika ujumbe wake, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa historia ya kimapinduzi na mapambano wakati wa zama za utawala wa taghuti na kisha kushiriki daima katika zama zote za Mapinduzi na kuchukua majukumu makubwa ya usimamizi wa nchi kama vile kuwa mkuu wa Idara ya Mahakama, uanachama katika Baraza la Walinzi wa Katiba, Baraza la Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na mjumbe katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) pamoja na harakati za kielimu na kifiqhi ni kati ya sifa za mwanazuoni huyo mwendazake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (kushoto) akiwa na marehemu Ayatullah Muhammad Yazdi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, imani thabiti kwa misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu, istiqama katika njia hii, kutetea dini na mapinduzi ni kati ya sifa zingine za wazi za mwanazuoni huyo.

Ayatullah Khamenei amemuomba Mwenyezi Mungu amrehemu amghufurie Ayatullah Muhammad Yazdi.

Maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametuma salamu zao za rambi rambi kufuatia kuaga dunia Ayatullah Muhammad Yazdi ambaye alizikwa jana mjini Qum.