Meja Jenerali Salami: Iran itatoa jibu kali kwa kitendo chochote cha adui
(last modified Sat, 02 Jan 2021 13:12:53 GMT )
Jan 02, 2021 13:12 UTC
  • Meja Jenerali Salami: Iran itatoa jibu kali kwa kitendo chochote cha adui

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) amesema: "Sisi tutajibu kitendo chochote cha adui kwa pigo kali".

Meja Jenerali Hussein Salami Kamanda Mkuu wa IRGC ameyasema hayo kwa mnasaba wa mwaka wa kwanza wa kukumbuka kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani wakati alipotembelea vikosi na vituo vya kijeshi katika Kisiwa cha BuMusa katika Ghuba ya Uajemi na kuongeza kuwa: "Luteni Jenerali Qassem Soleimani alipelekea maadui washindwe katika njama yao ya kubadilisha ramani ya ulimwengu wa Kiislamu. Aidha alipelekea maadui wa umma wa Kiislamu wakiwemo Marekani na hasa utawala wa Kizayuni washindwe wazi wazi".

Ameongeza kuwa maadui ambao walikuwa wanawaunga mkono magaidi wakufurishaji na hasa kundi la Daesh au ISIS walipata pigo kubwa kutokana na ushujaa wa Shahidi Soleimani.

Meja Jenerali Soleimani akiwa katika kisiwa cha BuMusa katika Ghuba ya Uajemi

Meja Jenerali Salami ameashiria stratijia ya ulinzi wa baharani ya IRGC katika kulinda visiwa vitatu hasa kisiwa cha BuMusa na kusema: "Visiwa vitatu vya BuMusa, Tomb Kubwa na Tomb Ndogo ni ardhi isiyotenganika ya Iran na ni ngome muhimu katika kulinda nchi mkabala wa maadui kutoka nje ya eneo."

Salami amesema utayarifu wa kivita katika visiwa hivyo ni wa uhakika na imara na kuongeza kuwa Iran haitaacha ipite vivi hivi hujuma yoyote ile itakayofanywa na adui pamoja na adui mwenyewe.