Brigedia Jenerali Hatami: Iran italipiza kisasi cha kuuawa shahidi Jenerali Suleimani
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kuwa, hakuna chembe ya shaka kuwa Jamhuri ya Kiislamu italipiza kisasi cha kuuawa kigaidi Shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani, aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).
Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema hayo leo katika Chuo cha Kijeshi mjini Tehran, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku alipouawa kigaidi na jeshi la Marekani, Haj Suleimani nchini Iraq.
Ameeleza bayana kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuata fikra, njia na tadubiri ya Shahidi Suleimani katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri.
Brigedia Jenerali Hatami amesema imeingiwa na wahakama na hofu ikisubiri kisasi cha damu ya Jenerali Suleimani, na ndipo imelazimika kuondoka katika eneo la Asia Magharibi.
Waziri wa Ulinzi wa Iran ameashiria kuhusu jitihada zinazofanywa na maadui ili kujaribu kudunisha ushawishi wa Iran katika eneo na kubainisha kuwa, nafasi athirifu ya Jamhuri ya Kiislamu inakwenda kinyume na mataifa mengine ya kieneo, ambayo yanadhani kuwa maslahi yao yatalindwa kwa kujidhalilisha na kujitweza kwa madola ajinabi.

Ikumbukwe kuwa, Januari 3 mwaka uliomalizika wa 2020, Luteni Jenerali Qassem Suleimani, Mkuu wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Harakati ya al Hashd al Shaabi na wanamapambano wenzao wanane, waliuliwa kigaidi na kidhulma na wanajeshi magaidi wa Marekani, katika shambulio la anga lililofanywa na magaidi hao karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.
Mauaji hayo ya kigaidi yaliyofanywa na wanajeshi vamizi wa Marekani yalilaaniwa si tu katika eneo hili la Asia Magharibi, bali kote duniani.