Iran kuzalisha kilo 9 za urani iliyorutubishwa kwa 20% kwa mwezi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65609-iran_kuzalisha_kilo_9_za_urani_iliyorutubishwa_kwa_20_kwa_mwezi
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) Ali Akbar Salehi amesema kuanzia sasa Jamhuri ya Kiislamu itakuwa inazalisha kilo tisa za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 kila mwezi.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jan 06, 2021 01:12 UTC
  • Iran kuzalisha kilo 9 za urani iliyorutubishwa kwa 20% kwa mwezi

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) Ali Akbar Salehi amesema kuanzia sasa Jamhuri ya Kiislamu itakuwa inazalisha kilo tisa za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 kila mwezi.

Salehi alisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, Iran imeanza kuzalisha gramu 17 hadi 20 za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 kwa saa, sawa na kilo 8 hadi 9 za bidhaa hiyo kwa mwezi, na hili litaendelea hadi pale nchi hii itakapofikia kilo zisizopungua 120 za urani hiyo kila mwaka kama ilivyoanishwa kwenye sheria.

Salehi amesema hayo pambizoni mwa marasimu ya kumkumbuka Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi mashuhuri wa nyuklia wa Iran, aliyeuawa shahidi  na utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 27 Novemba mwaka uliopita katika mji wa Abesard, mkoani Tehran.

Ameongeza kuwa, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran linaendelea kufanya shughuli zake kama kawaida, na hivi sasa linaunda vituo viwili vya nishati ya nyuklia huko Bushehr, kwa thamani ya dola bilioni 10.

Kituo cha nyuklia cha Fordow, kilichoko kaskazini mashariki mwa mji wa Qum kusini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran

Mapema jana pia, Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa alisema hatua ya Iran kuanza urutubishaji wa urani kwa asilimia 20 ni sehemu ya kupunguza uwajibikaji wake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, likiwa ni jibu kwa hatua za kiuhasama za Marekani dhidi ya Iran na kimya cha nchi za Ulaya mkabala wa hatua hizo za kiuadui. Araqchi amesisitiza kuwa, kitendo hicho cha Iran hakina maana ya kufa au kusambaratika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Marekani ilijiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA mwaka 2015 na kuanza kutekeleza vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hatua ambayo iliilazimisha Tehran ianze kupunguza hatua kwa hatua uwajibikaji wake katika mapatano hayo ya kimataifa.

Kadhalika usiku wa kuamkia jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif alisema hatua iliyochukulia na Jamhuri ya Kiislamu ya kuanza urutubishaji wa urani kwa asilimia 20 inaweza kuangaliwa upya, iwapo pande zote za JCPOA zitaheshimu na kufungamana na mapatano hayo kikamilifu.

Dakta Zarif akifafanua jambo