Zarif: Iran itakabiliana na hatua zisizo za kisheria za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i6583-zarif_iran_itakabiliana_na_hatua_zisizo_za_kisheria_za_marekani
Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameshiriki katika kikao cha wabunge wateule wa bunge la 10 la Iran na kutoa hotuba kuhusu maudhui ya "Utunguaji Sheria, Mahitajio na Mbinu".
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 07, 2016 08:22 UTC
  • Zarif: Iran itakabiliana na hatua zisizo za kisheria za Marekani

Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameshiriki katika kikao cha wabunge wateule wa bunge la 10 la Iran na kutoa hotuba kuhusu maudhui ya "Utunguaji Sheria, Mahitajio na Mbinu".

Katika hotuba yake, Zarif amesema kwa kuzingatia hali iliyoko, moja kati ya vipaumbele vya bunge jipya ni kuhakikisha nchi za Magharibi zinatekeleza ipasavyo mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) . Zarif amesema baadhi ya nchi zimeingiwa na wasi wasi baada ya Iran kuondolewa vikwazo. Hii ni kwa sababu baadhi ya makundi na nchi zimekuwa zikiendeleza sera zao kwa msingi wa kueneza chuki dhidi ya Iran na leo pia zinataka kuiarifisha Iran kama hatari katika eneo.

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje yamekuja kufuatia hatua za kiuadui za Marekani dhidi ya Iran baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia yaliyaoanza kutekelezwa mwezi Januari mwaka juu.

Sera zilizo dhidi ya Iran za Marekani zinatekelezwa katika duru kadhaa na zikiendelea basi zitakuwa na taathira hasi.

Alkhamisi, Gholamali Khoshro balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa alimkabidhi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa taarifa kutoka kwa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM. Taarifa hiyo ambayo imesajiliwa kama waraka rasmi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imeashiria suala la uhasama huo wa Marekani. Katika taarifa hiyo, imesisitizwa kuwa hatua ya Marekani kupora fedha za Benki Kuu ya Iran ni kinyume cha sheria na jambo hilo linaweza kuvuruga uthabiti katika uhusiano wa kimataifa na kudhoofisha utawala wa sheria kimataifa.

Ikumbukwe kuwa tarehe 20 Aprili, Mahakama Kuu ya Marekani ilipitisha uamuzi kuwa, katika kuchunguza madai ya waathirika wa eti makosa ya jinai za ugaidi mahakama za nchi hiyo zinaweza kutumia mali na fedha za Iran zilizozuiliwa nchini humo ili kuwalipa fidia watu hao. Mahakama hiyo ilisema dola bilioni mbili za Iran zilizo katika benki za Marekani zipewe familia za wanajeshi wa Marekani waliouawa mwaka 1983 katika hujuma ya bomu huko Beirut Lebanon ambayo Iran inatuhumiwa kuhisika nayo. Iran imekana vikali kuhusika na hujuma hiyo na kusema fedha ambazo mahakama ya Marekani imezichukua ni mali ya Benki Kuu ya Iran.

Hatua ya kuchukua udhibiti wa fedha za Iran zilizokuwa zimezuiliwa katika benki za Marekani mbali na kuwa ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa pia ni kinyume na mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani, Marekani ikiwemo.

Iran imelalamikia vikali hatua hiyo ya Marekani na hatua zingine za nchi hiyo katika kuvuruga mfumo wa kifedha na kibiashara baina ya Iran na nchi zingine duniani.

Kama ambavyo Waziri wa Mambo ya Iran alivyosisitiza, Iran ina haki ya kuchukua hatua za kisheria ili kupata haki zake na kulinda maslahi ya watu wa Iran mbele ya vitendo vinavyokiuka sheria vya Marekani.

Kuvuruga mfumo wa kifedha na kibenki na kupuuza ahadi zake za kimataifa si hatua pekee zilizochukuliwa na Marekani katika uga wa kimataifa.

Marekani pia imekuwa ikiingilia kazi za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA jambo ambalo limelalamikiwa mara kadhaa na Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowowte NAM.

Hivi sasa kuna wasi wasi kuwa Marekani itapiga mnada kinyume cha sheria mali za Iran zilizoko nchini humo.

Tamko la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na pia taarifa ya Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote ambayo wanachama wake ni karibu robo tatu ya jamii ya kimataifa ni jambo linaloashiria namna nchi nyingi duniani zinavyochukizwa na siasa za Marekani na pia ni dalili ya udharura wa kukabiliana na hatua haribifu za Marekani katika uga wa kimataifa.