Zarif: Muqawama wa Wairani umefelisha mashinikizo ya juu ya Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema muqawama, mapambano na kusimama kidete wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu kumeipigisha mweleka sera ya mashinikizo ya juu kabisa ya Marekani dhidi ya taifa hili.
Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana katika kikao cha wazi cha Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kuongeza kuwa: Leo (jana) ni siku ya mwisho ya urais wa Donald Trump nchini Marekani, ambapo sera ya utawala huo ya mashinikizo ya juu kabisa imefeli kwa msaada wa wananchi shupavu wa Iran.
Ameeleza bayana kuwa, taifa hili kwa kutumia vyombo vya sera zake zilizo wazi za nje pamoja na msaada wa wananchi, limeweza kukabili sera za uhasama za maadui.
Dakta Zarif amebainisha kuwa, hata vyombo vya habari vya kimataifa vinatambua kuwa sera ya mashinikizo ya juu kabisa ya Marekani imegonga mwamba kutokana na muqawama wa wananchi na diplomasia ya busara ya nchi hii.
Hivi karibuni pia, Rais Hassan Rohani alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itavuka salama kipindi kigumu cha vikwazo vya kidhalimu na vinavyokiuka sheria vya maadui kwa msaada wa taasisi zote za utendaji na msaada wa wananchi.
Utawala wa Trump uliofika ukingoni umekuwa ukitumia vikwazo na mashinikizo kwa lengo la kujaribu kulipigisha magoti taifa la Iran, lakini wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu wamesimama kidete katika kipindi chote mkabala wa uadui huo.