Iran yalaani hatua ya Wazayuni, yaonya juu ya kuangamizwa kabisa Palestina
-
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imelaani hatua ya Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel, Knesset, ya kuidhinisha muswada unaoweka udhibiti wa utawala huo ghasibu katika Ukingo wa Magharibi na Bonde la Jordan.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imetoa taarifa ikilaani hatua ya Bunge la Israel ya kuidhinisha muswada wa sheria ya kudhibiti Ukingo wa Magharibi na Bonde la Jordan na kusema: "Hatua hii ya Bunge la Knesset ni ishara nyingine ya kupenda kujitanua na chuki za utawala ghasibu wa Israel."
Taarifa hiyo inasema: “Hatua ya Bunge la Kizayuni, iliyochukuliwa sambamba na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na kuendelea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, inafichua zaidi kuliko wakati mwingine wowote ukweli kwamba, utawala huo hauna lengo lolote ghairi ya kuangamiza kabisa Palestina kama ardhi, taifa na utambulisho huru, na kwamba haujali maazimio yote ya Umoja wa Mataifa."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekumbusha majukumu ya kisheria, kimaadili na kisiasa ya nchi na mashirika ya kimataifa ya kulisaidia taifa la Palestina kupata haki ya kujitawala na kulikomboa kutoka kwenye uvamizi na ubaguzi wa rangi, na kusisitiza kuwa, upuuzaji wa jamii na taasisi za kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yao ya kukomesha mauaji kimbari na uhalifu wa kivita unaofanyika Gaza na katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan utapelekea kushadidi jinai za utawala huo.
Iitakumbukwa kuwa, siku ya Jumatano iiliyopita Bunge la Israel liliidhinisha rasimu ya muswada kuhusu udhibiti wa Ukingo wa Magharibi na Bonde la Jordan kwa kura 71 kati ya jumla ya kura 120. Kupasishwa muswada huo ni hatua nyingine ya kutaka kuunganisha maeneo hayo ya Palestina na ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.