Jenerali Salami: Sanaa ya IRGC ni kuyavunja madola ya kiistikbari
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema kazi kubwa ya jeshi la SEPAH ni kuyavunja na kuyasambaratisha madola ya kiistikbari.
Meja Jenerali Hussein Salami amesema hayo katika mkutano wake uliofanyika kwa njia ya intaneti na makamanda wa vikosi mbalimbali vya majeshi ya Iran na kubainisha kuwa, "kutokana na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu inayojumuisha utawala wa wanaodhulumiwa na kuvunja uistikbari, madola yenye nguvu duniani yamefanya kila yawezalo kuzuia kuchomoza nguvu hii mpya na muundo wake."
Jenerali Salami ameongeza kuwa: Bado tuna vita vikubwa mbele yetu, adui angalipo; ingawaje amenyauka, lakini bado ana hatari na amekataa kata kata kusalimu amri.

Ameashiria kuwa, IRGC ni mtumishi wa taifa la Iran na muasisi wa kuyapatia ufumbuzi matatizo ya watu, na kwamba wananchi wa Iran kamwe hawajawahi kuliacha jeshi hilo pweke katika nyakati zote zikiwemo za shida.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, madhali kuna mawasiliano, mashauriano na uhusiano wa karibu baina ya IRGC, wananchi wa Iran na serikali, basi hakuna dola lolote duniani linaloweza kuishinda Jamhuri ya Kiislamu.
Meja Jenerali Salami ameongeza kuwa, taifa hili litaendelea kusimama kidete mkabala wa uhasama na mashinikizo ya maadui.