Khatibzadeh: Huu si wakati mwafaka wa kuitishwa kikao cha JCPOA
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa, kwa kutilia maanani misimamo na hatua za karibuni za nchi tatu za Ulaya na Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaona kuwa huu si wakati mwafaka wa kufanyika kikao kisicho rasmi kilichopendekezwa na Mkuu wa Siasa za Nje za Umoja wa Ulaya baina ya nchi hizo na Tehran kuhusu kadhia ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Saeed Khatibzadeh amesema kuwa hadi sasa hakujashuhudiwa mabadiliko ya aina yoyote katika misimamo na mienendo ya Marekani, na serikali ya Joe Biden si tuu kwamba haijatupilia mbali sera za Donald Trump za mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Iran, bali pia haijatangaza azma ya kutekeleza majukumu yake jumla katika mapatano hayo ya nyuklia na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Khatibzadeh ameongeza kuwa: Suala la kila upande kutekeleza majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA halihitaji mazungumzo wala mjadala.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema Marekani inapaswa kukomesha vikwazo vyake haramu na vya upande mmoja na itekeleze majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na suala hili halihitaji mazungumzo wala azimio la Baraza la Usalama.
Saeed Khatibzadeh ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itajibu vitendo kwa vitendo na itajibu hatua na miendo ya kihasama ya adui kwa vitendo na mienendo mfano wake.
Hata huvyo amesisitiza kuwa, Iran itaendelea kushauriana na nchi wanachama wa sasa wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA na pia Mkuu wa Siasa za Nje za Umoja wa Ulaya, Josep Borrell.
Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif alisema kuhusu pendekezo lililotolewa na Borrell la kushirikishwa Marekani katika kikao cha kujadili JCPOA kwamba Iran haitafanya kikao chochote rasmi na Marekani kwa sababu nchi hiyo si mwanachama katika makubaliano hayo ya nyuklia.