Iran yaionya Israel dhidi ya kuchukua hatua yoyote ghalati
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i67570-iran_yaionya_israel_dhidi_ya_kuchukua_hatua_yoyote_ghalati
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuchukua hatua yoyote ghalati kwa kisingizio cha mripuko uliotokea katika meli ya utawala huo katika Bahari ya Oman wiki iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 06, 2021 04:44 UTC
  • Iran yaionya Israel dhidi ya kuchukua hatua yoyote ghalati

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuchukua hatua yoyote ghalati kwa kisingizio cha mripuko uliotokea katika meli ya utawala huo katika Bahari ya Oman wiki iliyopita.

Majid Takht-Ravanchi ametoa indhari hiyo Ijumaa ya jana katika barua yake kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, Israel itabeba dhima ya matokeo mabaya iwapo itafanya mahesabu mabaya kwa kisingizio cha mripuko huo.

Amesema tukio la kuripuliwa meli hiyo ya Israel ni sehemu ya mchezo wa kuigiza na operesheni za utawala huo ghasibu kwa shabaha ya kufikia malengo yao haramu.

Katika barua yake kwa Guterres, mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesema jamii ya kimataifa haipaswi kupotoshwa na bwabwaja hizo za Wazayuni wanaokusudia kuficha jinai na ukandamizaji wao hususan dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina; na jinai za utawala huo katika maeneo mbalimbali dunia hususan Asia Magharibi, kwa uingiliaji wa kijeshi.

Meli ya Israel iliyoripuka katika Bahari ya Oman

Haya yanajiri wiki moja baada ya meli ya mizigo ya utawala pandikizi wa Israel kuharibiwa katika mripuko uliotokea katika Bahari ya Oman. Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu bila kutoa ushahidi wowote, aliharakisha kudai kuwa Iran imehusika na mripuko huo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai hayo ya Wazayuni ambayo hayana msingi.