Iran yakanusha kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i67968-iran_yakanusha_kufanya_mazungumzo_yasiyo_ya_moja_kwa_moja_na_marekani
Duru za kiusalama nchini Iran zimekadhibisha madai ya Marekani kwamba kuna mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea baina ya Tehran na Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2021 01:00 UTC
  • Iran yakanusha kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani

Duru za kiusalama nchini Iran zimekadhibisha madai ya Marekani kwamba kuna mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea baina ya Tehran na Washington.

Duru hizo zilizo karibu na Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Iran zimenukuliwa na kanali ya Press TV zikisema kuwa, hakuna mazungumzo ya kidiplomasia yasiyo rasmi yanayoendelea kama alivyodai Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani.

Duru hizo za kiusalama za Iran zimebainisha kuwa, madai hayo ya kuwepo mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja juu ya mpango wa Marekaini kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA yameibuliwa ili kumuondoa Rais Joe Biden wa nchi hiyo katika kinamasi na mgogoro.

Chanzo hicho cha kiusalama kimeongeza kuwa, mamlaka na maafisa wote wa Iran wamefungamana na utekelezaji wa sheria iliyopasishwa na Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Mpango Kistratajia wa Bunge la Iran wa Kukabiliana na Vikwazo).

Chanzo hicho kimesema hakuna mazungumzo yoyote yatakayofanyika baina ya Tehran na Washington hadi vikwazo vyote vya kidhalimu dhidi ya taifa hili viondolewe.

Hivi karibuni pia, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haitofanya tena mazungumzo kuhusu mapatano ya kimataifa ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji kwa kifupi JCPOA, na kwamba Tehran inaishauri Washington ichukue haraka hatua za kuimarisha mapatano hayo kabla ya kutoweka fursa iliyopo.