Bri. Jen. Hatami: Uingereza ichukue hatua za kivitendo kulipa deni la Iran
Waziri wa Ulinzi wa Iran ameashiria jinsi Uingereza ilivyokiri kuwa ina deni la miaka 42 la Iran na kuitaka London ichukue hatua za kivitendo za kuilipa Tehran fedha zake hizo ambazo ni mamia ya mamilioni ya dola.
Brigedia Jenerali Amir Hatami alitoa mwito huo jana Jumanne na kuongeza kuwa, Uingereza inapaswa kuchukua hatua za kivitendo kutekeleza yale inayakiri na kuyasema kwa maneno.
Amesema Uingereza imekuwa ikikwepa kulipa deni hilo kwa visingizio visivyo na maana kama vile vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, jambo hilo limezidi kuharibu mtazamo wa taifa la Iran kwa Uingereza.
Matamshi ya Brigedia Jenerali Hatami ni radimali kwa kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Ben Wallace katika mahojiano na idhaa ya Times Radio ambapo amesisitiza haja ya London kuilipa Iran deni hilo.
Wallace amekiri katika mahojiano hayo kwamba, Uingereza ina deni la miaka 42 la Iran la pauni milioni 400 (dola milioni 551) na kuongeza kuwa London inapaswa kulipa deni hilo.
Deni hilo ambalo Iran inaidai Uingereza linahusiana na mkataba wa kuiuzia Iran vifaru 1500 vya Chieftain na magari 250 ya deraya ambayo London ilitiliana saini na utawala wa zamani wa Iran katika miaka ya 1974 na 1976.
UK haikuikabidhi Iran vifaru na magari hayo ya deraya kama ilivyoahidi, hata baada ya Mohammad Reza Pahlavi kupinduliwa madarakani mwaka 1979.