Iran yalaani hujuma za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Quds tukufu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali uvamizi na chokochoko mpya za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika mji mtukufu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Saeed Khatibzadeh amesisitiza kuwa, kuna haja ya utawala huo haramu kusitisha mara moja hujuma zake hizo dhidi ya wakazi wa Baitul Muqaddas zilizoanza tangu Alkhamisi iliyopita.
Kadhalika amevipongeza vikosi vya muqawama kwa ushujaa wao na hatua ya Wapalestina hususan wakazi wa Quds tukufu kusimama kidete kukabiliana na jinai hizo za Wazayuni.
Khatibadeh ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kukomesha vitendo vya jinai na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala pandikizi wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina wasio na ulinzi na maeneo matukufu.
Aidha Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kitendo cha Wazayuni kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kubainisha kuwa, Israel ni utawala pandikizi na njia pekee ya kutatua mgogoro wa Palestina-Israel ni kuitisha kura ya maoni katika eneo lote la Palestina.