May 16, 2021 04:32 UTC
  • Zarif afuta safari yake Austria akipinga kuwekwa bendera za Israeli kwenye majengo ya serikal

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amefuta safari yake rasmi nchini Austria akipinga hatua ya nchi hiyo ya kupeperusha bendera za utawala haramu wa Israel juu ya majengo ya serikali katika mji mkuu wa nchi hiyo Vienna, huku Israel ikiendelea kuwaua kinyama raia wa Palestina.

Stephanie Lajinstein, mwandishi wa habari wa Austria, alitangaza jana Jumamosi kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba, safari ya Muhammad Javad Zarif imesitishwa dakika ya mwisho kwa sababu ya kuwekwa bendera za Israel juu ya majengo ya ofisi za serikali.

Kabla ya hapo Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi alikuwa ameikosoa Austria kwa kupeperusha bendera za Israel juu ya majengo ya ofisi za serikali katika mji, Vienna, ambao ni mwenyeji wa mazungumzo muhimu yenye lengo la kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya nchi za Magharibi na Iran.

Araqchi aliitaja Vienna kuwa ni "mwenyeji mzuri wa mazungumzo" lakini akasema kuwa, hatua hiyo ya Austria "inashangaza na kuumiza" wakati huu ambapo utawala wa Israel unaendelea kuua idadi kubwa ya watu wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa kwa miaka kadhaa sasa.

Araqchi ameandika katika mtandao wa Twitter kwamba: "Inashangaza na kuumiza kuona bendera ya utawala unaoikalia Palestina kwa mabavu ikipepea juu ya ofisi za serikali mjini Vienna, utawala ambao umewaua kikatili makumi ya raia wasio na hatia, wakiwamo watoto wengi kwa siku chache tu." 

Watoto wa Gaza...

Kansela wa Austria, Sebastian Kurz hapo awali alikuwa ametoa pole kwa utawala wa Israeli na kuamuru kuwekwa bendera za utawala huo haramu juu ya ofisi za serikali katika mji mkuu.

Hatua hiyo ya Kansela wa Austria imechukuliwa kinyume na maandamano yalifanyika mapema wiki hii yakiwaunga mkono Wapalestina mjini Vienna. Waandamanaji hao walipinga vikali na kulaani mashambulizi ya mabomu, makombora na ndege za kivita ya utawala wa Tel Aviv dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza na ukatili wa Israel katika maeneo mengine ya Palestina.

Tags