Iran: Mgogoro wa Syria utamalizwa kwa kura za wananchi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, mgogoro wa Syria utamalizwa kwa kura na matakwa ya wananchi wenyewe wa Syria.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Sadegh Hossein Jaberi Ansari, akisema hayo jana (Jumamosi) wakati wa shughuli za kumkumbuka shahid Mustafa Badruddin hapa Tehran na kuongeza kuwa: Tangu awali kabisa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa inaamini kwamba, njia za kisiasa ndiyo pekee itakayotatua mgogoro wa Syria na mara nyingi imekuwa ikisisitiza kuwa, njia za kijeshi haziwezi kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Jaberi Ansari amesema kuhusu kutumwa askari wa nchi za kigeni huko Syria kwamba, madola ya kigeni yasiyoipendelea kheri Syria yataendelea kuingilia masuala ya nchi hiyo, maadamu njia za kisiasa hazijafuatwa kuutatua.
Amesema, serikali ya Syria imeiomba serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iwe inaitumia washauri wa kijeshi kila inapoiomba na hayo ni kwa mujibu wa makubaliano ya nchi mbili hizi.
Vile vile ametumia fursa hiyo kutoa mkono wa pole kwa taifa la Lebanon kufuatia kuuawa shahidi Mustafa Badruddin, kamanda wa muqawama wa Kiislamu huko nchini Syria na kuongeza kwamba: Ni jambo la kawaida kuona viongozi wakubwa kama hao wanauawa shahidi katika njia ya haki kwani kuuawa shahidi ndiyo sunna ya muqawama wa Kiislamu.