Siri ya kubakia hai Jamhuri ya Kiislamu katika mtazamo wa Kiongozi Muadhamuu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa ubunifu mkubwa zaidi ya hayati Imam Ruhullah Khomeini ni Jamhuri ya Kiislamu, kwa maana ya demokrasia ya kidini ambayo imetambulika rasmi kwa anwani ya Jamhuri ya Kiislamu na kwa anwani ya mfumo wa utawala uliojengeka kwa fikra za taifa la Iran na uongozi wa Imam Khomeini.
Ayatullah Khamenei ambaye jana Ijumaa lihutubia taifa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mwaka wa 32 tangu Imam Khomeini alipoaga dunia, amesema kuwa, siri kubwa ya kubakia hai Jamhuri ya Kiislamu nbini Iran imo katika maneno mawili "Jamhuri" na "Uislamu".
Wakati mfumo wa utawala wa Kiislamu ulipoasisiwa nchini Iran zaidi ya miaka 40 iliyopita maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu walikuwa wakisema utawala huo utatoweka na kusambaratika haraka, lakini hii leo uko katika mwaka wake wa 43 ukipiga hatua kubwa za maendeleo na mafanikio katika nyanja mbalimbali. Mshikamano wa wananchi na utawala wao katika nyanja mbalimbali za kisiasa hususan ushiriki wao mkubwa katika chaguzi mbalimbali katika kipindi chote cha miaka 42 iliyopita ndiyo nguzo ya kuendelea kuwepo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuzimwa njama mbalimbali za maadui. Ni mshikamano huu wa wananchi na kushirikishwa kwao katika ngazi zote za kuchukua maamuzi na vilevile kutegemea dini ya Uislamu ndiko kunakoyatofautisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi yaliyofanyika maeneo mengine ya dunia. Ukweli huu ndio unaoashiriwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei pale aliposema: Baadhi ya mapinduzi yalianza kwa hamasa ya kutia moyo na matumaini, lakini yalikuwa na mwisho wa kuhuzunisha.
Katika kipindi cha zaidi ya miongo minne iliyopita Jamhuri ya Kiislamu imepiga hatua kubwa za maendeleo katika nyanja mbalimbali licha ya vizuizi na vizingiti vingi ilivyokabiliana navyo. Mwenendo huu endelevu unaonesha kuwa, wakati wote wananchi, hususan tabaka la vijana, wanapokuwa katika medani na wakautambua Uislamu kuwa ndiyo mizani na kigezo cha maamuzi yao yote, basi matatizo yote yanaweza kuondoka na kutatuliwa kirahisi.
Hii leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kuvuka vikwazo na mashinikizo ya juu kabisa ya kisiasa na kupata mafanikio makubwa katika nyanja za sayansi, tiba, teknolojia ya kisasa, elimu za masuala ya anga, na zaidi ya yote imefanikiwa kuzalisha chanjo kadhaa za kukabiliana na virusi vya corona tena kwa kutegemea wasomi wake vijana.
Kwa sasa Iran inasubiri tukio jingine muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nalo ni uchaguzi ujao wa Rais na Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji; uchaguzi ambao daima umekuwa dhihirisho la kushirikishwa wananchi katika maamuzi muhimu ya kitaifa. Naam, wananchi ni nguzo muhimu sana ya kubakia hai Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na daima wamekuwa na nafasi muhimu katika demokrasia ya kidini ya Iran.
Pamoja na hayo, jambo lenye umuhimu mkubwa zaidi, kama alivyosema Ayatullah Ali Khamenei kwenye hotuba yake ya kumbukumbu ya kuaga dunia hayati Imam Khomeini, ni kuchagua viongozi sahihi na wanaofaa; suala ambalo litasaidia sana katika kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya matatizo ya kiuchumi.
Ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi ujao wa rais mbali na kudhihirisha mshikamano wa wananchi na utawala wao, vilevile utakuwa na taathira kubwa katika misimamo ya nchi ajnabi na katika mienendo yao mbele ya Jamhuri ya Kiislamu.