Iran yaonya dhidi ya misimamo hasi ya wakala wa IAEA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71022-iran_yaonya_dhidi_ya_misimamo_hasi_ya_wakala_wa_iaea
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika asasi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna Austria ametahadharisha kuhusu misimamo hasi na ya uhasama ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya Tehran.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 07, 2021 23:09 UTC
  • Iran yaonya dhidi ya misimamo hasi ya wakala wa IAEA

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika asasi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna Austria ametahadharisha kuhusu misimamo hasi na ya uhasama ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya Tehran.

Kazem Gharib Abadi ametoa indhari hiyo mapema leo Jumanne na kusisitiza kuwa, misimamo hiyo haribifu ya IAEA yumkini ukauweka hatarini uhusiano wa wakala huo wa Umoja wa Mataifa na Jamhuri ya Kiislamu katika siku sijazo.

Ameeleza bayana kuwa, "misimamo ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), Raphael Grossi umeonesha wazi mtazamo wa upande mmoja wa sekritarieti ya wakala huo kwa (hali) ya ushirikiano na Iran, na upuuzaji wa kiwango cha uhusiano wa pande mbili."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amebainisha kuwa, misimamo hiyo hasi ya IAEA mkabala wa Iran inaweza kuwa kizingiti katika njia ya mahusiano ya pande mbili hapo baadaye.

Raphael Grossi

Jana Jumatatu Grossi alidai kuwa, uwezo wa wakala huo wa kuweza kufuatilia 'malengo ya amani' katika miradi ya nyuklia ya Iran unaweza kuathiriwa vibaya na kile alichokitaja kuwa 'ukosefu wa maendeleo' katika kujibu masuali ya wakala huo kuhusu shughuli za nyuklia za taifa hili.

Alidai pia kuwa Jamhuri ya Kiislamu haijatekeleza ahadi zake za kushirikiana na wakala huo wa kimataifa wa niashati ya nyuklia. Kikao cha mwezi huu wa Juni cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kilianza jana Jumatatu.

Madai ya Grossi yameibuiliwa katika hali ambayo, ripoti zote za wakala wa IAEA zinaonyesha kuwa, hakuna ushahidi unaothibitisha kwamba, miradi ya nyuklia ya Iran imekengeuka mkondo wa amani.