Iran yaishauri Marekani iachane na turathi zilizofeli za Trump
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ingali inaamini kuwa ni jambo linalowezekana kufikia makubaliano katika mazungumzo ya kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA huko Vienna, iwapo utawala wa sasa wa Marekani utaamua kuweka pembeni sera na turathi zilizogonga mwamba za aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Donald Trump.
Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Jumamosi katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kubainisha kuwa, Tehran kutokana na kufungamana kwake kwa dhati na kuheshimu saini iliyotia kimataifa, hadi sasa inasalia kuwa mshiriki amilifu zaidi wa mazungumzo hayo ya Vienna.
Ameeleza bayana kuwa, katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu inafanya juu chini ya kuyahuisha mapatano hayo ya kimataifa, watawala wa Marekani kwa upande wao wanajipinda kila namna kuyasambaratisha.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, akthari ya rasimu zilizowasilishwa kwenye mazungumzo ya Vienna zimetayarishwa na ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu, ithibati tosha kuwa Iran imejitolea kwa dhati kuiokoa JCPOA.
Kadhalika amebainisha kuwa, inayumkinika kuyahuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA kwa sharti kwamba Marekani iachane na sera zilizofeli za Trump, na kwamba 'katu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitajihusisha na mazungumzo yasiyo na kikomo."