Mazungumzo baina ya Waafghani; njia pekee ya kutatua matatizo na changamoto zilizopo
Mazungumzo ya pande tatu kati ya jumbe za Afganistan na Iran yamefanyika mjini Tehran kwa madhumuni ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa nchi hiyo kwa kutegemea mazungumzo baina ya makundi tofauti ya nchi hiyo.
Huku akibainisha kupitia ujumbe wa Twitter kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama bega kwa bega na watu wa Afghanistan kwa ajili ya kutafuta amani ya kudumu chini humo, Dakta Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika kwamba wizara yake siku ya Jumatano ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo ya kirafiki na muhimu baina ya wawakilishi wa ngazi za juu wa Afghanistan.
Ujumbe wa kisiasa wa Afghanistan uliongozwa katika mazungumzo ya Tehran na Yunus Qanuni, waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Afghanistan nao ujumbe wa kundi la Taliban ukaongozwa na Abbas Stanikzai, naibu mkuu wa ofisi ya kundi hilo.
Ikiwa ni nchi jirani na iliyo na mpaka mrefu na Afghanistan, Jamhuri ya Kiislamu Iran inafuatilia kwa karibu matukio ya nchi hiyo na hili linatokana na umuhimu kwamba watu wa nchi mbili hizi wana masuala mengi ya pamoja na yanayofanana yakiwemo ya kiutamaduni, kilugha na kidini.
Uhusiano mzuri uliopo kati ya mataifa haya, maingiliano na safari nyingi zinazofanywa na Waafghani nchini Iran pamoja na uwepo wa miongo minne wa wakimbizi na wahijiri wa Kiafghani katika ardhi ya Iran, ni jambo linalowafanya Waafghani waichukulie Iran kuwa nchi yao ya pili.
Hilo ni moja ya mambo ambayo yameifanya Iran ifuatilie kwa karibu matukio ya Afghanistan na kuwa na nia njema ya kutaka kutatua matatizo ya kisiasa na kiusalama ya nchi hiyo kupitia mazungumzo ya Tehran.
Mwaliko wa Iran kwa jumbe zote husika za Afghanistan katika mzungumzo hayo unathibitisha wazi lengo na nia njema ya Iran katika kuheshimu maslahi ya kisiasa ya pande zote za Afghanistan.
Iran inaamini kwamba mazungumzo na utatuzi wa kisiasa wa matatizo ya Afghanistan ndiyo njia bora na ya pekee ya kutatua matatizo na kudhamini maslahi ya makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo jirani. Ni kwa msingi huo ndipo serikali ya Iran ikaandaa mazungumzo ya Tehran ili kujaribu kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya makundi tofauti ya Afghanistan na hatimaye kutatua kabisa mgogoro wa nchi hiyo.
Kama alivyosisitiza Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, hivi sasa baada ya kuondoka katika ardhi ya Afghanistan wanajeshi vamizi wa kigeni hakuna kizuizi kingine chochote kinachozuia makundi ya kisiasa ya nchi hiyo kuketi kwenye meza moja ya mazungumzo kwa ajili ya kutayarisha na kuwasilisha ramani ya njia itakayokidhaminia kizazi cha baadaye cha nchi hiyo mustakabali bora, wenye amani na ustawi.
Kwa kutilia maanani maslahi ya makabila tofauti ya Afghanistan, kuna umuhimu wa wawakilishi wa makundi hayo kushirikishwa katika matukio yote ya kisiasa na kiusalama ya Afghanistan, na hivyo kushiriki wawakilishi wa kundi la Taliban katika mazungumzo ya Tehran kunaweza kutathminiwa katika mtazamo huo.
Makundi ya kisiasa ya Afghanistan yalidhurika kwa njia moja au nyingine na uwepo wa askari ya kigeni katika ardhi ya nchi hiyo na makabila ya nchi hiyo hayaiamini kabisa Marekani. Ukweli huo unatoa umuhimu mkubwa wa makundi tofauti ya Afghanistan kushiriki katika mazungumzo ya amani yanayoandaliwa na marafiki halisi wa nchi hiyo na hasa Jamhuriya Kiislamu ya Iran, ili kujenga Afghanistan iliyoendelea na yenye amani na usalama wa kudumu. Ni kwa msingi huo ndipo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akayataja mazungumzo ya makundi tofauti ya Afghanistan mjini Tehran kuwa yenye umuhimu mkubwa.
Makundi yote ya kisiasa ya Afghanistan yanaamini kwamba njia za amani zilizojikita kwenye mazungumzo baina ya Waafghani ndiyo njia pekee ya utatuzi wa matatizo na changamoto za nchi hiyo kwa ajili ya kufikia utulivu wa kudumu na ruwaza iliyo wazi kwa ajili ya watu wa Afghanistan.