Zarif: Marekani inaficha uhalifu wake kwa kuzitupia tuhuma nchi nyingine
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i72440-zarif_marekani_inaficha_uhalifu_wake_kwa_kuzitupia_tuhuma_nchi_nyingine
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu propaganda chafu mpya za Marekani ndhidi ya Iran na kuishauri Washington ishughulikie masuala ya ndani ya nchi hiyo badala ya kuzitupia tuhuma nchi nyingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 16, 2021 22:40 UTC
  • Zarif: Marekani inaficha uhalifu wake kwa kuzitupia tuhuma nchi nyingine

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu propaganda chafu mpya za Marekani ndhidi ya Iran na kuishauri Washington ishughulikie masuala ya ndani ya nchi hiyo badala ya kuzitupia tuhuma nchi nyingine.

Muhammad Javad Zarif jana Ijumaa alijibu tuhuma mpya za Marekani dhidi ya Iran kwa kuashiria jinsi Washington ilivyohusika katika mauaji ya Rais wa Haiti na vilevile njama za nchi hiyo za kutaka kumuua Rais wa Vinezuela na kuandika katika mtandao wa Twitter kwamba: Mamluki wenye silaha wa Marekani wanapanga njama za kuwaua kigaidi viongozi wa nchi za Haiti na Venezuela katika ardhi ya Marekani, huku Washington ikifanya jitihada za kuficha mahusiano yake ya vitendo vya uhalifu kwa kuzitupia lamawa na tuhuma nchi nyingine kwamba zinahusika na utekaji nyara wa watu; madai ambayo ni kichekesho na ni ya kitoto. 

Muhammad Javad Zarif ameishauri Marekani kushughulikia hali yake ya ndani badala ya kuzituhumu nchi nyingine. 

Hivi karibuni Wizara ya Sheria ya Marekani ilitoa taarifa ikidai kuwa, polisi wa FBI wamezima jaribio la Iran la kutaka kuteka nyara mwanaharakati mmoja katika ardhi ya Marekani. 

Tehran imeyataja madai hayo ya Washington kuwa ni kichekesho na kwamba ni juhudi za serikali ya Washington za kutaka kuhuisha, bila ya matumaini, vibaraka na mamluki wake walionyong'onyea na kupoteza thamani.