Khatibzadeh: Iran iko tayari kutekeleza makubaliano ya kubadilishana wafungwa
(last modified Sun, 18 Jul 2021 08:06:12 GMT )
Jul 18, 2021 08:06 UTC
  • Khatibzadeh: Iran iko tayari kutekeleza makubaliano ya kubadilishana wafungwa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu madai ya viongozi wa Marekani akisisitiza kuwa: Iran leo iko tayari kutekeleza makubaliano ya kubadilishana wafungwa.

Saeed Khatibzadeh ameashiria makubaliano ya Iran na Marekani na Uingereza kuhusu kubadilishana wafungwa 10 kutoka pande zote kwa misingi ya kibinadamu na kwa uhuru na kueleza kuwa: Iran iko tayari leo hii kutekeleza makubaliano hayo. Khatibzadeh ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Inashangaza kuona Marekani inakanusha uhakika mwepesi kwamba, kumefikiwa mapatano kuhusu mahabusu hao ikiwa ni pamoja namna ya kulitangaza wazi suala hilo.  

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria mazungumzo ya Vienna na kueleza kuwa: Kumefikiwa mapatano huko Vienna na Marekani na Uingereza kuhusu suala la kubadilishana wafungwa, mbali na mazungumzo kuhusu mapatano ya JCPOA . 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imedai kuwa Washington itakuwa tayari kuendelea na mazungumzo ya Vienna baada ya kipindi cha kukkabidhiana madaraka nchini Iran. Wizara hiyo imeongeza kudai kuwa, Washington ilikuwa tayari kuendeleza mazungumzo lakini eti Wairani waliomba kupatiwa muda zaidi ili kumalizika kipindi cha kukabidhiana madaraka.  

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imetoa madai hayo masaa machache baada ya Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na mkuu wa timu ya Iran katika mazungumzo ya JCPOA kusisitiza katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: Suala la kubadilishana wafungwa limekuwa mateka wa malengo ya kisiasa.  

Sayyid Abbas Araqchi