Iran: Tumejitosheleza katika uzalishaji wa ndege zisizo na rubani (drone)
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii imefikia hatua ya kujitosheleza kikamilifu katika uzalishaji wa ndege zisizo na rubani (drone).
Afshin Khajeh-Fard ambaye anasimamia Shirika la Viwanda vya Anga la Iran alisema hayo jana Alkhamisi katika mahojiano na shirika la habari la IRNA, pambizoni mwa jukwaa la Iran katika Maonyesho ya Kimataifa ya Anga ya Russia MAKS 2021.
Amesisitiza kuwa, "tumepiga hatua kubwa katika uwanja huu (wa uzalishaji) wa droni, na mafanikio haya yamepatikana kutokana na jitihada kubwa zisizo na kikomo za vijana wetu shupavu katika kipindi cha zaidi ya miongo minne."
Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran ameeleza bayana kuwa, hii leo Jamhuri ya Kiislamu imejitosheleza katika uzalishaji wa droni, kuanzia kwa utengenezaji wa vipuri hadi injini za ndege hizo zisizo na rubani.
Mwezi Mei mwaka huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilizindua mafanikio matatu makubwa ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC ikiwemo droni (ndege isiyo na rubani) ya Ghaza.
Hivi karibuni, Jenerali Kenneth McKenzie, Kamanda wa Kamandi Kuu ya askari wa kigaidi wa Marekani CENTCOM, alikiri kwamba nguvu ya droni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepunguza na kudhoofisha pakubwa uwezo wa anga wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).