Kamanda Salami: Mipaka ya Iran ina usalama na ulinzi wa kutosha
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i73470-kamanda_salami_mipaka_ya_iran_ina_usalama_na_ulinzi_wa_kutosha
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amelithibitishia taifa la Iran kuwa mipaka ya mashariki ya nchi hii ipo salama.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 13, 2021 13:09 UTC
  • Kamanda Salami: Mipaka ya Iran ina usalama na ulinzi wa kutosha

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amelithibitishia taifa la Iran kuwa mipaka ya mashariki ya nchi hii ipo salama.

Meja Jenerali Hossein Salami amesema hayo leo Ijumaa katika mazungumzo yake na waandishi wa habari jijini Mashhad, kaskazini mashariki mwa nchi na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hii vipo macho na vinalinda kwa nguvu zote mipaka na vivuko vya upande wa mashariki mwa nchi. 

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo baada ya kuibuka wasi wasi na taharuki kutokana na matukio ya kiusalama yanayoshuhudiwa hivi sasa katika nchi jirani ya Afghanistan.

Meja Jenerali Salami amesema, "Wananchi (wa Iran) hawapaswi kuwa na wasi wasi kwa kuwa kina cha ufuatiliaji wetu kimevuka nje ya mipaka na tunafuatilia na kutathmini kwa karibu yale yanayojiri katika nchi jirani."

Wapiganaji wa Taliban

Tangu miezi takriban mitatu iliyopita, kufuatia tangazo la Marekani la kuondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan, kundi la Talban limeshadidisha mashambulio na kuyateka maeneo mengi ya ardhi ya nchi hiyo.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh sanjari na kueleza wasi wasi wake juu ya mapigano yanayoendelea baina ya wanamgambo wa kundi hilo na vikosi vya serikali ya Kabul katika pembe mbalimbali za Afghanistan, amesema usalama na afya ya wanadiplomasia vinapaswa kupewa kipaumbele.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh