Zarif: Iran itaendeleza jitihada za kusaidia kupatikana amani Afghanistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza jitihada za kuhakikisha kuwa amani na maridhiano yanapatikana nchini Afghanistan.
Muhammad Javad Zarif alisema hayo jana Jumapili katika ujumbe aliotuma kwenya ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Ghasia na vita-kama vile ukaliaji wa mabavu wa ardhi-katu havitatui matatizo."
Amesema Iran inakaribisha tangazo la rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai la kuundwa Baraza la Uratibu na viongozi wa Afghanistan; na kuongeza kuwa Tehran inatumai kuwa hatua hiyo itapelekea kufanyika mazungumzo na makabidhiano ya madaraka kwa amani nchini humo.
Dakta Zarif amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kusaidia na kufanikisha mazungumzo kati ya makundi ya Waafghani kwa lengo la kusogeza mbele mchakato wa amani huko Afghanistan.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, matatizo ya Afghanistan yanaweza kupatiwa ufumbuzi kupitia mazungumzo tu.
Katika hatua nyingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kukutana leo Jumatatu katika kikao cha dharura cha kujadili hali ya Afghanistan. Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan ameondoka nchini humo na kuelekea Tajikistan huku kundi la Taliban likitangaza kuwa limedhibiti taasisi zote za serikali katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul.
Weledi wengi wa mambo wanasema kuwa, hali ya sasa ya Afghanistan ni matokeo ya kufeli siasa za Marekani iliyoivamia nchi hiyo na kwa miongo miwili sasa.