Iran yatangaza uungaji mkono wake kwa taifa la Afghanistan
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, vivyo hivyo itaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Afghanistan na matakwa yao.
Ali Shamkhani amesema hayo leo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamiii wa twitter ambapo ameashiria matamshi ya kusikitisha ya Waziri wa Ulinzi wa Afghanistan na kubainisha kuwa: Kauli hiyo imeonesha athari za miaka 20 za ukaliaji wa mabavu wa ardhi ya Afghanistan uliofanywa na Marekani.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, "Katika safari yangu ya Kabul Disemba 2018, nilikuwa na mkutano wenye changamoto na Rais wa Afghanistan. Kama tulivyofanya miaka 40 iliyopita, tunawaunga mkono wananchi wa Afghanistan na irada yao."
Hapo jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza jitihada za kuhakikisha kuwa amani na maridhiano yanapatikana nchini Afghanistan.
Muhammad Javad Zarif alisema hayo katika ujumbe aliotuma kwenya ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "Ghasia na vita-kama vile ukaliaji wa mabavu wa ardhi-katu havitatui matatizo."
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kukutana leo Jumatatu katika kikao cha dharura cha kujadili hali ya Afghanistan.
Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan ameondoka nchini humo na kuelekea Tajikistan huku kundi la Taliban likitangaza kuwa limedhibiti taasisi zote za serikali katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul.