Khatibzadeh: Iran itatumia uwezo wake kuleta maelewano Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i73600-khatibzadeh_iran_itatumia_uwezo_wake_kuleta_maelewano_afghanistan
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatumia uwezo wake wote kwa ajili ya kuhimiza mazungumzo na maelewano nchini Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 17, 2021 04:02 UTC
  • Khatibzadeh: Iran itatumia uwezo wake kuleta maelewano Afghanistan

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatumia uwezo wake wote kwa ajili ya kuhimiza mazungumzo na maelewano nchini Afghanistan.

Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh Jumatatu na huku akiashiria matukio ya nchi hiyo jirani amesema: "Tunafuatilia kwa karibu matukio ya Afghanistan na tunawasiliana na wahusika wote."

Amesema kama ambavyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alivyosema katika ujumbe wa Twitter, Iran inakaribisha pendekezo la rais wa zamani wa Afghanistan Hamid Karzai kuhusu kuundwa baraza la uratibu nchini humo.

Khatibzadeh amesema Iran na Afghanistan zina nukta nyingi za pamoja za kihistoria na kiutamaduni na kwamba Iran daima imekuwa ikisimama pamoja na taifa la Waislamu la Afghanistan katika nyakati muhimu za historia. 

Rais Muhammad Ashraf Ghani wa Afghanistan aliyetoroka nchi

Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina wasi wasi kuhusu machafuko nchini Afghanistan na inatoa wito kwa pande zote kudumisha amani kupitia mazungumzo.  

Wapiganaji wa kundi la Taliban, Jumapili Agosti 15 waliingia mji mkuu wa Afghanistan, Kabul sambamba na kuanguka kwa serikali kufuatia hatua ya Rais Muhammad Ashraf Ghani kuitoroka nchi.