Rais wa Iran amemteua Eslami kuwa Mkuu mpya wa AEOI
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemteua Mohammad Eslami kuwa Mkuu mpya wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (AEOI).
Katika dikrii iliyotolewa jana Jumapili, Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Iran amemteua Eslami kuja kurithi mikoba ya Ali Akbar Salehi.
Eslami alikuwa Waziri wa Barabara na Ustawi wa Miji na Majiji katika serikali iliyopita ya 12 ya Dakta Hassan Rouhani.
Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran AEOI ni moja ya taasisi muhimu na hasasi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikisisitiza kuwa, katika hali ambayo taifa hili lina haki ya kuendelea kustafidi na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani na kiraia, lakini msimamo usiobadilika wa Iran ambao unaenda sanjari na fatua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba, ni haramu kumiliki silaha za nyuklia.
Tehran inasisitiza kuwa, haijaunda wala kamwe haitaunda bomu la atomiki, kwani uundaji, umiliki na utumiaji wa silaha hizo angamizi unakwenda kinyume na mafundisho wa Uislamu.