Amir-Abdollahian: Iran iko tayari kuiuzia Lebanon mafuta zaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuendelea kuiuzia serikali na wafanyabiashara wa Lebanon mafuta.
Hussein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Ijumaa katika mazungumzo yake ya simu na Gebran Bassil, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon na kuongeza kuwa: Iran haina kizuizi cha kupanua uhusiano wake na Lebanon na iko tayari kuwauzia wateja wapya mafuta yake.
Amesema stratejia iliyopasishwa na kiongozi wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa ajili ya kutamatisha mgogoro wa mafuta uliobuniwa na Wazayuni dhidi ya wananchi wa Lebanon imeonesha wazi kuwa, heshima na hadhi ya Lebanon itapatikana tu kwa kujitegemea taifa hilo na kutumia mali na rasilimali zake.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran itaendelea kuisaidia na kuiunga mkono serikali ya Lebanon, jeshi na kambi ya muqawama ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Hii ni katika hali ambayo, meli ya kwanza ya mafuta ya Iran juzi Alkhamisi iliingia katika maji ya Syria, ambapo inatazamiwa kupakua shehena za mafuta zitakazosafirishwa kuelekea Lebanon kwa kutumia usafiri wa malori ya mafuta.
Baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutuma meli ya kwanza ya mafuta kuelekea Lebanon Agosti 19; Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah alionya kuwa, uchokozi wowote utakaofanywa dhidi ya meli hiyo utakuwa ni uchokozi dhidi ya ardhi ya Lebanon.