Maelfu ya wakimbizi wa Kiafghani wanaingia Iran kila siku
Shirika moja la Ulaya la kushughulikia maslahi ya wakimbizi limeiasa jamii ya kimataifa kuwapa msaada wa chakula na makazi maelfu ya wakimbizi wanaoingia nchini Iran kila siku wakitokea Afghanistan.
Jan Egeland, Katibu Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway ametoa mwito huo baada ya kuutembelea mkoa wa Kerman, uliopo katika mpaka wa nchi hii na Afghanistan.
Amesema, baada ya kundi la Taliban kutwaa madaraka nchini Afghanistan, maelfu ya Waafghani wameitoroka nchi yao na kuingia nchini Iran. Egeland ameeleza kuwa, tangu Taliban iingie madarakani mnamo Agosti mwaka huu, raia zaidi ya laki tatu wamekimbia Afghanistan.
Katibu Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway amebainisha kuwa, aghalabu ya wakimbizi wa Kiafghani wamesema kuwa wana azma ya kuelekea Ulaya na hivyo ameiasa Ulaya kutoshughulishwa sana na wakimbizi wachache waliokwama katika mpaka Poland na Belarus, kwani wanaoingia nchini Iran ni wengi mno.
Amesema wakati wa msimu wa baridi kali, malaki ya wakimbizi wengine wanatazamiwa kuondoka Afghanistan na kukimbilia nchini Iran.
Kuna wakimbizi zaidi ya laki nane wa Kiafghani waliosajiliwa nchini Iran, na wengine zaidi ya milioni tatu ambao hawajasajiliwa rasmi.
Afisa huyo amesema Iran haipaswi kuendelea kubebea mzigo wa wakimbizi pekee, na kwamba Ulaya ina jukumu la kuwekeza katika matumaini, uwezeshaji na fursa ndani ya Afghanistan iwapo haitaki kushuhuhudia wimbi la wakimbizi katika bara hilo.