Jan 29, 2022 03:21 UTC
  • Amir-Abdollahian: Iran haijafanya mazungumzo yoyote ya moja kwa moja na Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran haijafanya mazungumzo yoyote ya moja kwa moja na Marekani.

Katika kikao na wajumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu  (Bunge la Iran) Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amewasilisha ripoti ya mchakato wa mazungumzo ya Vienna katika fremu nne za kuondolewa Iran vikwazo, kutekelezwa ahadi za nyuklia, kupata dhamana na utaratibu wa kuhakikisha ahadi zinatekelezwa.

Katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje amebainisha kuhusu jitihada zinazofanywa na Ali Baqeri, kiongozi wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya Vienna pamoja na ubunifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo hayo na kusema: "Iran ina irada ya kufikia mapatano mazuri, endelevu na yenye kutegemewa."

Amir-Abdollahian ameendelea kusema kuwa, ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Vienna haujafanya mazungzo yoyote ya moja kwa moja na Marekani. Ameendelea kusema kuwa, mitazamo ya kiufundi ya pande mbili imekuwa ikiwasilishwa kwa njia ya maandishi yasiyo rasmi na kupitia mratibu wa Umoja wa Ulaya.

Mazungumzo ya Vienna baina ya Iran na kundi la 4+1

Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna, ambayo ajenda yake kuu ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na visivyo vya kisheria ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilianza mwishoni mwa mwaka uliomalizika.

Mazungumzo hayo ni baina ya Iran na kundi la 4+1 ambalo linazileta pamoja Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Russia na China pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya.

Marekani ambayo ilijiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018 iliiwekea Iran vikwazo haramu kufuatia uamuzi wake huo na kusababisha mkwamo kwenye utekelezaji wa mapatano hayo, inashiriki mazungumzo ya Vienna nchini Austria kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Tags