Iran yaikosoa Marekani kwa kuibua maudhui mpya katika mazungumzo ya Vienna
(last modified Sun, 13 Mar 2022 07:58:03 GMT )
Mar 13, 2022 07:58 UTC
  • Iran yaikosoa Marekani kwa kuibua maudhui mpya katika mazungumzo ya Vienna

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameijia juu Marekani kwa kuibua maudhui nyingine mpya kwenye mazungumzo ya Vienna kati ya Jamhuri ya Kiislamu na kundi la 4+1, ambayo lengo lake kuu ni kuondolewa Tehran vikwazo vya kidhalimu.

Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Qatar ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo ya Kiarabu, Sheikh Abdul Rahman Al Thani; ambapo walijadili uhusiano wa pande mbili, na masuala ya kieneo sanjari na mazungumzo ya Vienna.

Amir-Abdollahian ameeleza kuwa, maombi mapya ya Marekani kwenye mazungumzo ya Vienna hayana mantiki wala uhalali wowote, na yanakinzana na madai ya Washington ya kutaka kufikiwa haraka mapatano.

Amesisitiza kuwa, Tehran inakaribisha juhudi zote za kuharakisha kufikiwa makubaliano mazuri, imara na ya kudumu kwenye mazungumzo ya Vienna, ambayo kwa sasa yamesimamishwa kwa muda.

Kabla ya hapo, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran alisisitiza kuwa, masuala ya msingi na kuondolewa Iran vikwazo havipaswi kuathiriwa na tabia ya kujitakia makuu Marekani.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Abdul Rahman Al Thani mbali na kusisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa pande mbili wa Doha na Tehran katika nyuga tofauti, amesema kuna haja ya kufanywa jitihada za makusudi katika mazungumzo ya Vienna, kwa shababa ya kufikiwa mapatano mazuri.