Iran: Tumeieleza wazi Marekani, hatuwezi kufumbia macho mistari yetu myekundu
(last modified Thu, 24 Mar 2022 07:11:56 GMT )
Mar 24, 2022 07:11 UTC
  • Iran: Tumeieleza wazi Marekani, hatuwezi kufumbia macho mistari yetu myekundu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran imeieleza wazi Marekani kuwa kamwe haiwezi kuvuka mistari yake myakundu.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo baada ya kuonana na kufanya mazungumzo na Faisal al Miqdad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria mjini Damascus na kuongeza kuwa, kama Marekani itaamiliana na mambo katika uhalisia wake, basi Iran nayo itakuwa tayari kufikia makubaliano karibuni tu hivi, kwenye kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa kamati ya pamoja ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesema, amefanya mazungumzo muhimu na mazuri sana na Rais Bashar al Assad wa Syria na Faisal Miqdad, waziri mwenzake wa mambo ya nje wa nchi hiyo kuhusu masuala ya nchi mbili, ya kieneo na ya kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran (kushoto) katika mazungumzo na Rais Bashar al Assad wa Syria mjini Damascus

 

Kabla ya hapo pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa amesisitizia ulazima wa kuzingatiwa maslahi ya taifa la Iran na mistari myekundu ya Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kikamilifu kufikia makubaliano mazuri, imara na endelevu ya nyuklia.

Hossein Amir-Abdollahian alisisitiza hayo katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Muhammad bin Abdurahman Aal Thani.

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje wa Qatar alipongeza mchango chanya wa Iran katika mazungumzo ya Vienna na akatilia mkazo ulazima wa pande zote kufanya juhudi za kufikia mwafaka haraka utakaokubaliwa na pande zote.