Ayatullah Khatami: Marekani isubiri vipigo zaidi vya kudhalilisha vya Iran
Khatibu wa Muda wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehrah ameashiria kugonga mwamba sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, Washington ijiandae tena kushindwa kunakodhalilisha na Iran mwaka huu.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo katika hotuba za leo za Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika ukumbi wa Imam Khomeini (MA) hapa Tehran na kuongeza kuwa, maafisa wenyewe wa Marekani wamekiri wazi wazi juu ya kufeli kampeni ya mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ametoa mwito kwa maafisa wa serikali ya Iran kuifanyia kazi kaulimbiu ya mwaka huu wa Kiirani ulioanza Machi 21, iliyotangazwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei inayosema: Uzalishaji; Wenye msingi wa Elimu, na Kubuni nafasi za Ajira.
Ayatullah Khatami amewaonya maafisa wa Marekani kwa kuwaambia wanapaswa wajiandae kwa vipigo zaidi vya kudhalilisha vya Iran.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema mashinikizo ya kiuchumi ni njia ambayo imekuwa ikitumiwa daima na maadui wa taifa hili, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kusimama kidete mkabala wa njama hizo.
Sayyid Ahmad Khatami ameongeza kwa kusema, anatumai maafisa wa serikali na viongozi wa Iran watawahudumia tena wananchi kwa moyo wa matumaini na kujitolea, baada ya kumalizika likizo fupi ya mwaka mpya wa Hijria Shamsia.