Iran: Vikosi vamizi vya Marekani viondoke Syria mara moja
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i81788-iran_vikosi_vamizi_vya_marekani_viondoke_syria_mara_moja
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema vikosi vya Marekani na waitifaki wake vinapaswa kuondoka Syria haraka iwezekanavyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2022 21:53 UTC
  • Iran: Vikosi vamizi vya Marekani viondoke Syria mara moja

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema vikosi vya Marekani na waitifaki wake vinapaswa kuondoka Syria haraka iwezekanavyo.

Majid Takht-Ravanchi alitoa mwito huo alipohutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa: Vikosi ajinabi vikiwemo vya Marekani vinatishia usalama na mamlaka ya kujitawala ya Syria, na vinapaswa kuondoka nchini humo mara moja pasi na masharti yoyote.

Amesema hali ya kibinadamu nchini Syria inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku, na hivi sasa kwa mujibu wa takwimu za UN, Wasyria milioni 14.6 wanahitaji misaada ya dharura ya kibinadamu.

Takht-Ravanchi ameeleza kuwa, kwa hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili Syria, maajinabi hawafanyi chochote kutafutia ufumbuzi hali hiyo, bali wanaifanya iwe mbaya zaidi, kwa kuzikalia kwa mabavu ardhi za nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.

Magari ya jeshi la Marekani yakiiba mafuta ya Syria

Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amelaani hatua ya magaidi wa jeshi la Marekani na vibaraka wao ya kupora mafuta, nafaka na rasilimali nyinginezo za Wasyria huko mashariki na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Kiarabu, na kubainisha kuwa wizi huo unakiuka wazi Hati ya Umoja wa Mataifa.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, mgogoro wa Syria hauwezi kumalizwa bila kukomesha ukaliaji wa mabavu wa ardhi ya nchi hiyo, sanjari na kukabiliana na magenge ya kigaidi.