Iran haiwezi kusalimu amri mbele ya kujitakia makuu Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu katu haiwezi kusalimu amri mkabala wa uchu, tamaa na kujitakia makuu Marekani.
Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema hayo jana Jumatatu katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa, Tehran inafanya maamuzi kwa izza na mantiki kwa ajili ya maslahi ya taifa hili, na daima inachunga mistari miekundu ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ameeleza bayana kuwa, Marekani inabeba dhima ya kusita na kuchukua muda mrefu mazungumzo ya Vienna ya kuiondolewa Iran vikwazo, kutokana na matakwa yake yanayochupa mipaka.
Amir-Abdollahian amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo tayari kwa ajili ya kufikia makubaliano mazuri na ya kudumu lakini Marekani inakwamisha jitihada za kufikiwa mapatano hayo.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha kuwa, iwapo Marekani itafuata mkondo wa uhalisia wa mambo, basi hakuna shaka makubaliano yatafikiwa tena katika kipindi kifupi.

Suala la kutoa hakikisho ili kuaminiwa, na kuwaondoa katika orodha yake nyekundu na katika safu ya vikwazo shakhsia wa kisheria lingali ni kati ya kadhia ambazo Marekani ikiwa upande uliokiuka mapatano ya JCPOA haijachukua maamuzi muhimu ya kisiasa kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa mara nyingine tena amekosoa hatua ya Marekani ya kuwawekea vikwazo vipya baadhi ya shakhsia na mashirika ya Jamhuri ya Kiislamu.