Iran: Ushirikiano wa kieneo ndio utaimarisha usalama Ghuba ya Uajemi
(last modified Fri, 15 Apr 2022 04:01:39 GMT )
Apr 15, 2022 04:01 UTC
  • Iran: Ushirikiano wa kieneo ndio utaimarisha usalama Ghuba ya Uajemi

Waziri wa Ulinzi wa Iran amelaani uwepo haramu wa madola ajinabi katika eneo la kistratajia la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz na kusisitiza kuwa, ushirikiano wa nchi za Asia Magharibi ndiyo dawa mjarabu ya kudhamini usalama na uthabiti wa eneo hili.

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo ya simu na Nobuo Kishi, Waziri wa Ulinzi wa Japan na kuongeza kuwa, sera ya ulinzi ya Iran inalipa uzito suala la kushirikiana nchi za eneo kwa ajili ya kujidhaminia usalama wao.

Amesema uwepo wa maajinabi katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz kinyume cha sheria ndio unaovuruga usalama wa eneo hili la kistratajia.

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani, Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema Japan na Jamhuri ya Kiislamu vina maeneo muhimu na hasasi ya kijiopolitiki upande wa mashariki na magharibi mwa Asia, na nchi mbili hizi zimeazimia kuimarisha uhusiano wao katika fremu ya kudhamini amani na uthabiti katika eneo kwa njia chanya.

Eneo la kistratajia la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz

Kwa upande wake, Nobuo Kishi, Waziri wa Ulinzi wa Japan sambamba na kugusia kuhusu harakati za vikosi vya majini vya nchi yake katika eneo la Asia Magharibi, amesisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano na Iran, ili kuhakikisha usalama wa baharini unakuwepo.

Machi mwaka huu, Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Admeri Alireza Tangsiri alisema usalama wa Lango Bahari la Hormuz  na Ghuba ya Uajemi vina umuhimu wa kistratejia katika mlingano wa kiusalama kimataifa na kieneo, na ndio maana hatua yoyote ya kujaribu kuvuruga usalama huo haiwezi kufumbiwa macho na Iran.