Wabunge wa Iran: IAEA imepoteza itibari ya kiufundi
(last modified Mon, 13 Jun 2022 10:58:40 GMT )
Jun 13, 2022 10:58 UTC
  • Wabunge wa Iran: IAEA imepoteza itibari ya kiufundi

Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) imesema hatua ya Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ya kupasisha azimio dhidi ya Iran imeonesha wazi kuwa taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imepoteza itibari yake ya kiufundi.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na wabunge 260 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumapili imesema azimio hilo dhidi ya Tehran lilipasishwa kisiasa na linakiuka mipaka.

Azimio hilo lilipendekezwa na Marekani pamoja na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na lilipasishwa Jumatano iliyopita na Bodi ya Magavana ya IAEA licha ya upinzani mkali wa China na Russia.

Taarifa ya wabunge hao wa Iran kadhalika imelaani safari ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) huko Israel na kueleza kuwa: Kwa bahati mbaya, Mkurugenzi Mkuu mwenyewe (wa IAEA) na sekritarieti ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hakuna shaka wamepoteza itibari yao ya kiufundi.

Watunga sheria wa Jamhuri ya Kiislamu wamebainisha kuwa, safari ya Grossi huko Israel, pamoja na ukweli kwamba utawala wa Kizayuni hautambui Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Atomiki NPT, ni ishara tosha kuwa Mkurugenzi Mkuu huyo wa IAEA ana mienendo inayoegemea upande mmoja.

Grossi na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

Wamesema hulka ya Grossi kutokuwa na msimamo madhubuti inatia shaka iwapo ataweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwenye taasisi hiyo, ambayo ni kuhakikisha kuwa silaha za nyuklia zinasambaratishwa.

Aidha wabunge hao wametangaza kuiunga mkono serikali ya Iran na Shirika la Nishati ya Atomiki la taifa hili katika kupunguza ushirikiano na wakala wa IAEA.