Mahujaji wa Kiirani walaani kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel
(last modified Sat, 09 Jul 2022 09:45:28 GMT )
Jul 09, 2022 09:45 UTC
  • Mahujaji wa Kiirani walaani kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel

Ummati mkubwa wa Mahujaji wa Kiirani sambamba na kutangaza uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina, lakini umekosoa pia njama ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sehemu ya taarifa iliyosomwa na Mahujaji hao wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakiwa katika viwanja vya Arafa jana Ijumaa inasema: Ukombozi wa Quds Tukufu kilipo Kibla cha kwanza cha Waislamu, kutoka kwenye mikono ya utawala unaotenda jinai wa Kizayuni na unaoua watoto, ni jambo la dharura na kipaumbele kwa umma wa Kiislamu.

Wametangaza uungaji mkono wao kwa taifa la kimuqawama la Palestina, sanjari na kulaani mpango wowote wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Hapo jana, Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia walisimama katika uwanja wa Arafa, kisimamo hicho kikiashiria kilele cha ibada tukufu ya Hijja. 

Katika sehemu nyingine ya taarifa yao, Mahujaji wa Iran wamezikosoa Marekani na utawala wa Kizayuni kwa kula njama za kupanda mbegu za chuki miongoni mwa Waislamu.

Kadhalika Mahujaji hao wa Jamhuri ya Kiislamu wameutaka umma wa Kiislamu kufungamana na mafundisho ya Qurani Tukufu na Mtume Muhammad SAW.