Jul 29, 2022 10:11 UTC
  • Mafuriko yameua watu tisa katika eneo la Firuzkuh, Tehran

Mkuu wa Mkoa wa Tehran amesema watu tisa ameuawa kufuatia mafuriko usiku wa kuamkia Ijumaa katika wilaya ya Firuzkuh iliyo katika milima ya mashariki mwa Tehran na kuongeza kuwa watu wengine 16 hawajulikani waliko na wengine 13 wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Muhsin Mansuri, Mkuu wa Mkoa wa Tehran  amesema mafuriko yalijiri katika wilaya ya Firuzkuh katika eneo la Hileh Rud na kupelekea watu tisa kufariki katika vijiji vya  Zarindasht, Mazdaran,na Atshan ambapo hadi sasa watu tisa wamethibitishwa kupoteza maisha na wengine 16 hawajulikani waliko.

Aidha amesema watu kumi waliokuwa wamejeruhiwa wamepata matibabu na kurejea nyumbani huku wengine wawili wakiwa wamelezwa hospitalini. Hali kadhalika amesema usiku wa kuamkilia Alhamisi kulikuwa na mafuriko katika eneo la Imam Zadeh Dawoud mjini Tehran na kupelekea watu wanane kupoteza maisha na wengine 19 bado hawajulikani waliko.

Eneo lililokumbwa na mafuriko

Mvua zisizo za kawaida zimekuwa zikishuhudiwa katika eneo la Asia Magharibi katika msimu huu wa joto kali mwaka huu ambapo zimeibua hasara kubwa ya maisha na mali.

Jana katika Umoja wa Falme za Kiarabu mvua kubwa zilizosababisha mafuruko zimeripotiwa katika eneo la Fujaira na zimetajwa kuwa mvua kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa eneo hilo katika kipindi cha miaka 30.

Nchini Pakistan karibu watu zaidi ya 300 wamepoteza maisha katika mafuruko ya hivi karibuni katika mji wa bandarini wa Karachi wenye idadi ya watu zaidi ya milioni 16.

Wataalamu wa mambo wanasema sababu ya mvua zisizo za kawaida zinazosababisha mafuriko ni kuharibiwa mazingira ambako kumepelekea kuwepo mabadiliko makubwa katika mfumo wa tabianchi.

Tags