Rais Raisi: Imam Khomeini (MA) aliwaamini wananchi
Rais Ebrahim Raisi amesema, mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kwa wananchi haukuwa mtazamo wa kiheshima tu, kwa sababu aliwaamini kiudhati wananchi na akisisitiza kuwa kutokana na imani juu ya Mwenyezi Mungu, kuwatumikia wananchi kunamfanya mtu awe karibu na Yeye Mola.
Seyyid Ebrahim Raisi ameyasema hayo mapema leo baada ya kuongoza mawaziri wake katika ziara ya kuzuru Haram ya Imamu Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba wa kuwadia maadhimisho ya Wiki ya Serikali kwa lengo la kuthibitisha tena baia na ahadi ya kuendeleza njia ya Kiongozi Mkuu huyo wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwa kusema: "leo tumekuja kuahidiana na Imamu Khomeini (MA) kwamba utumishi wetu utakuwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu" na akaongezea kwa kusema: "serikali inaitakidi kuwa popote pale inapowategemea wananchi inafanikiwa."

Raisi ameeleza pia kwamba sababu ya Iran kupata ushindi katika vita vya Kujihami Kutakatifu ni imani aliyokuwa nayo Imam Khomeini kwa wananchi na akasisitiza kwa kusema: mtazamo huo wa Imamu inapasa uwe ndio dira na mwongozo wa kufuata.
Halikadhalika, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa uadilifu inapasa uzingatiwe na kupewa umuhimu na viongozi wote wa serikali, kwani kama zitapigwa hatua katika muelekeo huo itawezekana kujenga imani kwa wananchi.../