Iran yakosoa mkutano wa NPT kwa kutoshinikiza Israel ijiunge na mkataba huo
(last modified Fri, 26 Aug 2022 03:55:58 GMT )
Aug 26, 2022 03:55 UTC
  • Iran yakosoa mkutano wa NPT kwa kutoshinikiza Israel ijiunge na mkataba huo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameukosoa vikali Mkutano wa Kumi wa Kuangalia Upya Maazimio ya Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kuziia Uzalishaji na Usambazi za Silaha za Nyuklia NPT unaofanyika huko New York, kwa kukataa kutoa mwito kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kujiunga na mkataba huo wa kimataifa.

Hossein Amir-Abdollahian katika mazungumzo yake ya simu na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, Rais wa mkutano huo, Gustavo Zlauvinen ameiondoa kwa makusudi kadhia ya kuishinikiza Israel ijiunge na NPT, kinyume na makongamano ya huko nyuma.

Amemhutubu Guterres kwa kusema: Kuweka pembeni mafanikio yote ya mikutano iliyopita ni jambo lisilokubalika kwa hali yoyote ile. Mkutano huo wa NPT ulioanza Agosti Mosi, unamalizika leo Ijumaa.

Amir-Abdollahian amesema utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unaungwa mkono na kukingiwa kifua na Marekani unapaswa kujiunga na Mkataba wa NPT na uheshimu sheria za kimataifa.

Mwanadiplomasia huyo amesema kitendo cha jamii ya kimataifa cha kufumbia macho silaha za nyuklia zinazomilikiwa na utawala dhalimu wa Israel ni hatari kwa usalama wa dunia nzima. Israel ndio utawala pekee ambao si mwanachama wa NPT katika eneo la Asia Magharibi licha ya kujilimbikizia silaha hatari za mauaji ya halaiki ya watu.

Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema Katibu Mkuu wa UN katika mazungumzo yake ya simu na Abdollahian ameeleza matumaini yake kuwa mazungumzo ya nyuklia ya Vienna yatazaa matunda.

Dujarric ameongeza kuwa, Guterres amesisitiza kuwa jitihada zilizofanywa na pande zote juu ya kuifufua JCPOA zina umuhimu mkubwa.