Sep 02, 2022 12:11 UTC
  • Khatibu wa Swala ya Ijumaa: Mkusanyiko wa Arubaini hauna mfano wake duniani

Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa hapa Tehran hii leo amesema, Arubaini ya Imam Hussein (AS) ndio mkusanyiko mkubwa zaidi wa wanadamu, na ambao ni wa aina yake na usio na mfano wake duniani.

Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesema hayo leo katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa hapa Tehran na kuongeza kuwa, matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) aidha ndiyo matembezi makubwa zaidi duniani.

Haj Ali Akbari ameashiria mjumuiko huo mkubwa zaidi wa watu ulimwenguni wa Arubaini ya Imam Hussein (AS) na kueleza kuwa, Arubaini ni harakati mashuhuri katika utamaduni wa kisiasa wa Iran na dunia.

Khatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa hapa Tehran ameongeza kuwa, Arubaini ndio harakati kubwa na mashuhuri zaidi dhidi ya ubeberu na uistikbari katika dunia ya leo.

Tarehe 17 Septemba 2022, itakayosadifiana na tarehe 20 Mfunguo Tano Safar 1444 Hijria itakuwa ni Arubaini ya siku aliyouawa shahidi Imam Hussein (AS), Imam wa Tatu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia duniani pamoja na masahaba zake waaminifu katika jangwa la Karbala.

Mkusanyiko wa Arubaini

Mamilioni ya wafanyaziara kutoka pembe zote za dunia ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huelekea mji wa Karbala kusini mwa Iraq ili kuhudhuria shughuli ya Arubaini ya Imam Hussein (AS).

Kwengineko katika hotuba zake, Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa katika ukumbi wa Mosalla ya Imam Khomeini (MA) hapa Tehran amegusia mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA, na kuziasa nchi za Ulaya kukumbatia fursa iliyopo ya kufidia na kusahihisha makosa yake mkabala wa mapatano hayo ya kimataifa.

Tags