Oct 23, 2022 12:50 UTC
  • Iran: Ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na ugaidi wa vyombo vya habari

Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran amesema, vyombo vya habari vyenye uadui vinapindua ukweli na kuandaa habari bandia ili kujaribu kutoa taswira isiyo sahihi kuhusu Iran ya Kiislamu na Ulimwengu wa Kiislamu.

Mohammad Mehdi Esmaili ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa kwa nyakati tofauti na shirika la utangazaji la Uturuki TRT na shirika la habari la Anadolu la nchi hiyo pia.

Esmaili ameeleza kuwa, Uislamu ni dini ya upendo na urafiki na akafafanua kwamba, maadui wanatoa taswira isiyo sahihi kuhusu Uislamu kwa kutumia habari bandia na simulizi potofu na kuwatangaza Waislamu kuwa ni magaidi, ilhali dini ya Uislamu ni mwenezaji wa watu kuishi pamoja kwa masikilizano, udugu na amani. 

Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu wa Iran ambaye alielekea Uturuki kushiriki mkutano wa 12 wa mawaziri wa habari wa nchi za Kiislamu ameongeza kuwa: kikao cha Istanbul kinaweza kutoa mwanga wa kuimarisha mawasiliano nchi za Kiislamu na kustawishwa zaidi mashirikiano baina yao na kuchangia katika kulinda utamaduni wa Kiislamu na umma mmoja wenye mapenzi na Mtume SAW na Watu wa Nyumba yake.

Esmaili ameashiria jinsi vyombo vya habari vya Magharibi vilivyoakisi matukio ya hivi karibuni nchini Iran na akasema: Iran ya Kiislamu imeandamwa na ugaidi wa vyombo vya habari; kwa sababu kila kona ya dunia kunajiri matukio mbalimbali ambayo yanafanywa yaonekane kuwa ni ya kawaida, lakini matukio yanayofanana na hayo yanapojiri Iran huakisiwa kwa kupindua ukweli na kutoa habari bandia ili kujenga taswira iliyo kinyume na uhalisia wa mambo.

Katika hotuba aliyotoa kwenye kikao cha mawaziri wa mawasiliano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kilichofanyika mjini Istanbul, Waziri wa Utamaduni wa Mwongozo wa Kiislamu wa Iran ametilia mkazo kuandaliwa mazingira ya ushirikiano wa pamoja kwa ajili ya kukabiliana na hujuma za kiutamaduni na ugaidi wa vyombo vya habari dhidi ya Ulimwengu wa Kiislamu.../

 

Tags