Tehran yaiasa China iheshimu visiwa vya Ghuba ya Uajemi, milki ya Iran
(last modified Mon, 12 Dec 2022 10:44:51 GMT )
Dec 12, 2022 10:44 UTC
  • Tehran yaiasa China iheshimu visiwa vya Ghuba ya Uajemi, milki ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameiasa China iheshimu mamlaka kamili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran juu ya visiwa vyake vitatu vya eneo la Ghuba ya Uajemi.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa lugha ya Kichina hii leo na kuongeza kuwa, visiwa vitatu hivyo vya Ghuba ya Uajemi ni sehemu ya milele ya ardhi ya Iran. 

Amesema: Visiwa vitatu vya  AbuMusa, Tunb Ndogo, na Tunb Kubwa ni sehemu zisizotenganishika na Iran, na daima vitasalia kuwa milki ya ardhi mama ya Iran. Abdollahian ameongeza kuwa: Iran haishughulishwi na pande nyinginezo ikija katika suala la udharura wa kuheshimiwa milki yake.

Mwandiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa visiwa hivyo vitatu vya Ghuba ya Uajemi ni sehemu za milele za ardhi ya Iran na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitafanya mazungumzo kuhusu mamlaka ya mipaka yake.

Ujumbe wa Twitter wa Abdollahian kwa lugha ya Kichina

Msimamo huo wa Amir-Abdollahian ni radiamali kwa taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya kikao  cha Rais wa China, Xi Jinping na viongozi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi katika mji mkuu wa Saudia wa Riyadh tarehe 9 Disemba. Taarifa hiyo ilipinga umiliki wa Iran wa visiwa vitatu vyake vya  AbuMusa, Tunb Ndogo, na Tunb Kubwa.

Hapo jana, Ali Nikzad, Naibu Spika wa Bunge la Iran sanjari na kusisitiza kuwa Tehran inamiliki visiwa hivyo vitatu alieleza kuwa, siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekuwa ni kutowatawala wengine na kutokubali kutawaliwa.

Maafisa wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba visiwa vitatu vya Abu Musa, Tunb Ndogo na Tunb Kubwa ambavyo Umoja wa Falme za Kiarabu unadai kuwa eti ni milki yake, ni sehemu ya ardhi yake.