Iran: Marekani ikhitari diplomasia badala ya mashinikizo na vitisho
(last modified Tue, 20 Dec 2022 07:48:16 GMT )
Dec 20, 2022 07:48 UTC
  • Iran: Marekani ikhitari diplomasia badala ya mashinikizo na vitisho

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema iwapo Marekani inataka kweli kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, haina chaguo jingine isipokuwa kukhitari njia ya diplomasia badala ya mashinikizo, vitisho na makabiliano.

Amir Saeed Iravani alisema hayo jana Jumatatu akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kilichojadili JCPOA na utekelezaji wa Azimio Nambari 2231 la baraza hilo linalohusu makubaliano hayo.

Irvani amebainisha kuwa, 'Hakuna shaka kuwa JCPOA inaweza tu kuhuishwa kwa kushughulikia mzizi na chimbuko la hali ya hivi sasa, ya Marekani kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa.

Makubaliano ya nyuklia ya Iran yalitiwa saini mwaka 2015 kati ya Tehran na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na China wakati wa uongozi wa Barack Obama.

Vikao vya Vienna vya kujaribu kuhuisha JCPOA

Hata hivyo, mrithi wa Obama, Donald Trump aliyachana makubaliano na JCPOA mwezi Mei 2018 na kuiwekea Iran vikwazo vya kikatili na vya upande mmoja.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameongeza kwa kusema: Mashinikizo, vitisho na makabiliano sio suluhu ya (kujaribu kufufua JCPOA) na havitaishia popote. Iwapo Marekani inataka kweli kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, sharti izingatie diplomasia.