Jan 03, 2023 15:21 UTC
  • Wananchi wa Iran wamkumbuka Jenerali Soleimani aliyeuawa kigaidi na Marekani

Wananchi kote katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo wametoa heshima kwa shujaa wao Jenerali Haj Qassem Soleimani, kamanda maarufu duniani wa mapambano dhidi ya ugaidi ambaye aliuawa katika hujuma ya kigaidi ya Marekani mwaka 2020.

Watu walikusanyika katika mji wa kusini-mashariki wa Kerman, mji alikozaliwa Jenerali Soleimani, ili kutoa heshima kwa kamanda huyo mashuhuri.

Maadhimisho kama hayo  yamefanyika pia katika mji mkuu wa Iran, Tehran, na miji mingine, ikiwa ni pamoja na Esfahan, Yazd, Birjand, Rasht, Shahr-e Kord na Arak.

Jenerali Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na msaidizi wake wa Iraq Abu Mahdi al-Muhandis, mkuu wa pili wa Kitengo cha Wapiganaji wa Kujitolea (PMU), waliuawa shahidi pamoja na wanajihadi wenzao katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani mnamo Januari 3, 2020.

Shahidi Soleimani

Hujuma hiyo karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad iliidhinishwa na rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump. Siku chache baada ya kuuawa shahidi, mwili wa kiongozi huyo wa kupambana na ugaidi ulihamishiwa Iran na kuzikwa katika mji aliozaliwa wa Kerman.

Makamanda hao wawili mashuhuri wa kupambana na ugaidi waliheshimiwa na kupendwa sana katika eneo zima kwa mchango wao mkubwa katika kupambana na kuliangamiza kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh au ISIS katika eneo, hususan katika nchi za Iraq na Syria.

Mapema wiki hii, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema Kamanda Soleimani aliitia nguvu za kimaada na kimaanawi kambi ya muqawama na kuyafanya mapambano yake dhidi ya utawala wa Kizayuni na ubeberu wa Marekani na nchi nyingine za kiistikbari yawe imara zaidi na ya kudumu milele.

Katika taarifa ya Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema mauaji ya kamanda mkuu wa kupambana na ugaidi ni "mfano dhahiri wa kitendo cha kigaidi kilichopangwa."

Taarifa hiyo imesema jinai ya kumuua Jenerali Soleimani, iliyotekelezwa na Marekani, ni mfano mwingine dhahiri wa 'ugaidi ulioratibiwa.'

Mauaji ya kigaidi ya Jenerali Soleimani yaliyotekelezwa na Marekani yalileta wimbi la kulaaniwa kutoka duniani kote na kusababisha maandamano makubwa duniani kote, huku wabunge wa Iraq wakiidhinisha muswada wa sheria siku chache baada ya shambulio hilo la Marekani na kutaka vikosi vyote vya kijeshi vinavyoongozwa na Marekani nchini Iraq vifurushwe.

Mnamo Januari 8, 2020, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ililenga kambi ya Ain al-Asad inayomilikiwa na Marekani katika mkoa wa magharibi wa Anbar nchini Iraq kwa wimbi la mashambulizi ya makombora kulipiza kisasi mauaji ya Jenerali Soleimani.

Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, zaidi ya askari 100 wa Marekani walipata "majeraha ya kiwewe ya ubongo" wakati wa shambulio hilo. IRGC ilisema Pentagon ilificha idadi ya askari wa Wamarekani waliouawa wakati wa kulipiza kisasi.

Iran imeelezea shambulio la kombora dhidi ya Ain al-Assad kama "kofi la kwanza".

 

Tags