Iran yamuita balozi wa Ufaransa kulalamikia uafriti wa 'Charlie Hebdo'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i92512-iran_yamuita_balozi_wa_ufaransa_kulalamikia_uafriti_wa_'charlie_hebdo'
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi wa Ufaransa mjini Tehran, Nicolas Roche kulalamikia vikali kitendo cha jarida la Kifaransa cha kutukana na kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu na thamani za kitaifa na kidini za Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2023 00:01 UTC
  • Iran yamuita balozi wa Ufaransa kulalamikia uafriti wa 'Charlie Hebdo'

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi wa Ufaransa mjini Tehran, Nicolas Roche kulalamikia vikali kitendo cha jarida la Kifaransa cha kutukana na kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu na thamani za kitaifa na kidini za Jamhuri ya Kiislamu.

Hivi karibuni, jarida la Charlie Hebdo lilifanya mashindano ya vibonzo vya kumvunjia heshima Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema katu Jamhuri ya Kiislamu haitoruhusu kuvunjiwa heshima thamani zake za kitaifa na kidini kwa kisingizio chochote.

Nasser Kan'ani amemkabidhi balozi huyo wa Ufaransa mjini Tehran barua rasmi ya malalamiko na kumtaka aiwasilishe kwa serikali ya Paris ili itoe maelezo na fidia kwa kitendo cha jarida hilo la Kifaransa cha kuvunjia heshima thamani za kidini na kitaifa za Iran.

Kan'ani amesema kitendo hicho cha kichochezi na kinachogusa nyoyo na hisia za mamilioni ya Wairani na Waislamu kote duniani hakipaswi kuhalalishwa kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.

Wairani katika maandamano ya kulaani uafriti wa Charlie Hebdo kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW

Hii si mara ya kwanza kwa jarida hilo linalochapishwa nchini Ufaransa kukanyaga thamani za kidini pamoja na uhuru wa imani na itikadi za watu wengine, kwa kuwatusi Waislamu na matukufu yao.

Jarida la Charlie Hebdo limeshapicha mara kadhaa katuni na vibonzo dhidi ya dini hususan dhidi ya dini tukufu ya Uislamu na Mtume wake Muhammad (S.A.W) kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, licha ya kukabiliwa na malalamiko makubwa ya Waislamu nchini Ufaransa na katika pembe mbalimbali za dunia.