Jan 15, 2023 03:29 UTC
  • Iran yalaani mauaji ya Mmarekani mweusi yaliyofanywa na polisi Los Angeles

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali mauaji ya kikatili ya raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika, yaliyofanywa na polisi ya nchi hiyo akisisitiza kuwa, Washington inapaswa kubebeshwa dhima ya wimbi la ukatili dhidi ya Wamarekani weusi.

Nasser Kan’ani amesema mauaji ya Keenan Anderson, mwalimu mweusi wa Marekani aliyekuwa na umri wa miaka 31 yametonesha kidonda na yanakumbusha kitendo cha kuuawa kinyama Mmarekani mwengine mwenye asili ya Afrika, George Floyd.

Ikumbukwe kuwa, mauaji hayo ya kikatili ya George Floyd mwaka 2020 baada ya kukandamizwa shingo na polisi Mzungu yalizusha maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi si tu Marekani, bali kote duniani. 

Kan'ani ameeleza bayana kwamba, mauaji ya mwalimu huyo mweusi kwa mara nyingine tena yamefichua na kudhihirisha sera za kibaguzi za Washington dhidi ya raia wa weusi wa nchi hiyo.

Mwalimu huyo ambaye ni binamu ya Patrisse Cullors, mwanzilishi wa harakati ya 'Black Lives Matter' iliyoshika kasi baada ya mauaji ya Floyd, ameaga dunia akitibiwa hospitalini huko Santa Monica, California, baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo uliotokana na kupigwa na bastola ya ganzi na maafisa wa polisi mjini Los Angeles.

Maandamano ya kulaani ukatili wa polisi ya US dhidi ya Wamarekani weusi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, utawala wa Marekani una misimamo ya kindumakuwili, kwani kwa upande mmoja unaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kwa maslahi ya kisiasa, na kwa upande mwingine, unafumbia macho ukatili, ubaguzi na jinai za polisi ya nchi hiyo dhidi ya Wamarekani weusi.

Utafiti wa karibuni wa Chuo Kikuu cha Washington ulibaini kwamba, Wamarekani weusi wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi wa kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi kuliko kundi lolote lingine katika jamii ya Marekani; na kwamba uwezekano wa Mmarekani mweusi kuuawa na polisi ni mara 3.5 zaidi kuliko Wamarekani weupe.

 

Tags